Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Virusi vya polio vyabainika Israel:WHO

Virusi vya polio vyabainika Israel:WHO

Virusi vya polio aina ya 1(WPV1) vimebainika katika sampuli za maji taka yaliyokusanywa April9 mwaka huu Kusini mwa Israel. Virusi hivyo vimebainika kwenye maji taka pekee hakuna tukio lolote la kupooza lililoripotiwa.

Uchunguzi unaendelea ili kujua chanzo cha virusi hivyo kwani uchunguzi wa awali umebaini kwamba virusi hivyo havina uhusiano na vile vinavyoathiri Pembe ya Afrika hivi sasa.

Virusi hivyo vilibainika wakati wa upimaji wa maji taka ambao hufanyika mara kwa mara Israel. Taifa hilo ,limekuwa huru bila virusi vya polio tangu mwaka 1988. Mara ya mwisho virusi hivyo vilibainika tena kwenye sampuli ya maji taka mwaka 1991 na 2002 lakini hakuna binadamu yeyote aliyeathirika.

Kufuatia hali hiyo shirika la afya duniani WHO limesema linafanya tathimini ya hatari ya kusambaa kimataifa virusi hivyo kutoka Israel. Limeongeza kuwa ni muhimu kwa nchi zote hususani kwa wale wanaosafiri mara kwa mara na kwenda kwenye mataifa yaliyoathirika na virusi vya polio kuwa makini zaidi. Mwaka 2013 Pembe ya Afrika imekumbwa na mlipuko wa polio huku visa sita vikiripotiwa Kenya na Somalia.