Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mizozo Afrika imepungua lakini kuna vitisho vipya vya amani na utulivu:Ban

Mizozo Afrika imepungua lakini kuna vitisho vipya vya amani na utulivu:Ban

Kusongesha mbele harakati za maendeleo kama msingi wa amani ni kauli ambazo nimetoa wakati nilipotembelea Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, DRC nikiambatana na Rais wa benki ya dunia, ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon wakati wa mjadala wa wazi kuhusu amani na utulivu kwenye kongamano la tano la Tokyo kwa maendeleo ya Afrika, TICAD-V mjini Tokyo. Bwana Ban amesema inamaanisha kuwekeza katika maendeleo ya kiuchumi huku juhudi za kuleta amani,usimamizi wa haki za binadamu na utawala wa kisheria zikiendelea baraniAfrika, ni jambo muhimu huku akipongeza hatua ya Japan ya kutoa dola Milioni 550 za kuendeleza amani na usalama barani Afrika. Amesema jitihada za namna hiyo zimefanya bara la Afrika hivi sasa liwe na idadi ndogo ya mizozo ikilinganishwa na awali, lakini vitisho vipya vinaibuka kama vile uhalifu unaovuka mipaka ya kitaifa, uharamia, ugaidi na itikadi kali za misingi mbali mbali akitaja mizozo ya Mali, Jamhiuri ya Afrika ya Kati na Ukanda wa Sahel. Katibu Mkuu Ban amesema bara la Afrika tayari lina mifumo mizuri ya kushughulikia migogoro akitoa mfano wa Mfumo wa kujitathmini utawala bora APRM. Hata hivyo amesema mashauriano ya kikanda na Jumuiya ya kimataifa katika kutatua mizozo ya Afrika na vitisho vipya  ni muhimu kwa amani na utulivu wa kudumu.