Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufanisi wa kudhibiti malaria wahitaji juhudi za kitaifa na ufadhili

Ufanisi wa kudhibiti malaria wahitaji juhudi za kitaifa na ufadhili

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ameliambia kongamano la tano

la kimataifa la Tokyo kuhusu maendeleo ya Afrika, TICAD kuwa ugonjwa

wa malaria ni janga la kibinadamu ambalo huzipokonya familia watoto

wao na kuzihuzunisha jamii, na hivyo ufanisi katika vita dhidi ya ugonjwa huo utahitaji nchi kuuvalia njuga na pia misaada inayotumika vyema. Bwana Ban amesema malaria huathiri chumi za kitaifa, na kwa sababu hiyo, ni lazima ugonjwa huo upewe kipaumbele kwenye ajenda ya kimataifa, hasa katika awamu hii ya mwisho ya msukumo wa kuyafikia malengo ya maendeleo ya milenia, na maendeleo baada ya 2015.  Bwana Ban amesema kwa kuongeza maradufu matumizi ya vyandarua vyenye dawa za kuua mbu Kusini mwa Jangwa la Afrika, vifo vitokanavyo na malaria vilipunguzwa kwa thuluthi moja. Amesema sasa ni wakati wa tahadhari, ambapo uhaba wa kifedha unatishia hatua za ufanisi zilizopigwa katika kukabiliana na malaria. Katibu Mkuu amesema huu ndio wakati wa kuhakikisha uwekezaji wenye matokeo, akisema kuwa mkakati wa Roll Back Malaria umethibitisha kuwa ushirikiano unaweza kuleta matokeo mema, kama vile Hazina ya Kimataifa ya Global Fund ilivyoonyesha kuwa usaidizi wa kutegemewa unahakikisha maendeleo.