Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban azungumza ana kwa ana na viongozi kadhaa wa Afrika mjini Yokohama, Japan

Ban azungumza ana kwa ana na viongozi kadhaa wa Afrika mjini Yokohama, Japan

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ambaye anahudhuria kongamano la tano la kimataifa la Tokyo kuhusu maendeleo ya Afrika, TICAD, amekutana na kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na viongozi kadhaa kutoka barani Afrika.

Miongoni mwa viongozi aliokutana nao ni mwenyekiti wa Muungano wa Afrika, Nkosazana Dlamini-Zuma, ambaye amebadilishana naye mawazo kuhusu matukio katika nchi kadhaa, zikiwemo Somalia, Madagascar, Mali, Sudan na Sudan Kusini, ukanda wa Maziwa Makuu na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mwngine alokutana naye ni Rais Boni Yayi wa Benin, aliyejadili naye kuhusu masuala ya kijamii na kiuchumi, pamoja na mipango ya uongozi mwema na kupiga vita ulanguzi wa madawa ya kulevya na uhalifu wa kupangwa.

Bwana Ban pia amekutana na Rais Alassane Ouattara wa Cote d'Ivore, ambaye amezungumza naye kuhusu hali nchini mwake, na nchi za Mali, Guinea na Afrika Magharibi kwa ujumla, akisifu hatua zilizopigwa nchini Cote d'Ivore na changamoto zilizopo bado, na kushukuru mchango wa Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS katika kutafuta amani nchini Mali.

Akikutana na Rais Idris Debi wa Chad, Bwana Ban na rais huyo wamejadili kuhusu masuala ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mali, eneo la Sahel, Libya, Sudan na Sudan Kusini, pamoja na tishio la wanamgambo wa Boko Haram.

Wengine alokutana nao ni Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegn, na rais wa mpito wa Mali,Dioncounda Traoré, rais wa Tunisia, Moncef Marzouki, na Waziri Mkuu wa Misri, Hesham Qandil,