Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usawa wa kijinsia na kumwezesha mwanamke wa Afrika kujadiliwa Tokyo:UNDP

Usawa wa kijinsia na kumwezesha mwanamke wa Afrika kujadiliwa Tokyo:UNDP

Umuhimu wa usawa wa kijinsia na kumuwezesha mwanamke katika kuchagiza maendeleo barani Afrika itakuwa ajenda kuu kwenye mjadala wa ngazi ya juu utakaoendeshwa na mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la maendeleoo UNDP Bi Helen Clark kwenye mkutano wa kimataifa wa maendeleo ya Afrika utakao anza Jumapili Tokyo Japan.UNDP inasema mjadala utajikita zaidi kwenye njia bora za kushughulikia changamoto kama afya ya uzazi, usalama wa chakula, ukatili wa kimapenzi, vikwazo vya kiuchumi kwa wanawake, uwezeshaji wa kisheria na kisiasa, pamoja na ushiriki wa wanawake katika kuleta amani.

UNDP pia imeainisha kwamba wanawake ndio wanaobeba jukumu kubwa katika kilimo ikikadiriwa kwamba karibu asilimia 50 ya nguvu kazi ya kilimo ni wanawake Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na asilimia kubwa zaidi katika sehemu zingine .

Imeongeza kuwa wanawake pia ndio wanaobeba mzingio wa kutafuta rasilimali za nishati katika jamii.  Suala la jinsia limeelezwa kuwa muhimu pia katika mazingira na sera za nishati ikiwemo kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Bi Clark amesema moja ya hatua muhimu ambazo nchi zinaweza kuchukua ni kuhakikisha na kuimarisha haki za kisiasa, kijamii na kiuchumi na kutoa fursa kwa wanawake. Akiongeza kuwa Afrika imepiga hatua kubwa katika kukuza uchumi hivi karibuni.Amesema kuhakikisha maendeleo endelevu lazima makundi yote katika jamii yajumuishwe na kuboresha maisha ya wanawake, wanaume na watoto.