Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yajiandaa kusaidia wakimbizi Sudan Kusini mvua zinapokaribia

UNHCR yajiandaa kusaidia wakimbizi Sudan Kusini mvua zinapokaribia

Nchini Sudan Kusini, shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR linaandaa misaada ya kibinadamu kwa ajili ya wakimbizi wakati huu ambapo msimu wa mvua umekaribia. George Njogopa anafafanua zaidi.

(RIPOTI YA GEORGE NJOGOPA)

Zaidi ya wakimbizi 190,000 kutoka Sudan kwa sasa wanaishi katika eneo la Unity na katika jimbo la Upper Nile lililoko Kaskazini mwa Sudan Kusini.

Katika eneo Unity ambako wanakutikana kiasi cha wakimbizi 73,097 ambao wengi wao wanaishi katika kambi ya Yida wanatarajiwa kufikiwa na misaada ya kibinadamu wakati wowote kuanzia wiki ijayo.Gari la mwisho lilobeba shehena ya misaada liliondoka mjini Juba siku ya alhamisi.

Mara itakapokamilia awamu ya mwisho ya usambazaji wa huduma hizo, hatua ya awali kwa ajili ya kusambaza huduma nyingine katika eneo la Unity inatazamiwa kuanza.

Mpaka May 26 mwaka huu, UNHCR inasema kuwa ilikuwa imeandikisha kiasi cha wakimbizi 378 katika Jimbo la Upper Nile wakati wakimbizi 92 waliandikishwa katika eneo la Unity.