China yawarejesha watoto kinguvu Korea Kaskazini

31 Mei 2013

Kundi la watoto tisa raia wa Korea Kaskazini waliokamatwa nchini Laos mapema juma hili wamerudishwa kwa lazima nchini mwao na serikali ya China kwa mujibu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa. Jason Nyakundi na taarifa kamili. (RIPOTI YA JASON NYAKUNDI)

Watoto hao walikabithiwa serikali ya  China baada ya kukamatwa walipojaribu kuingia nchini Laos. Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa inasema kuwa kuna hofu kuwa huenda watoto hao wakakabiliwa na dhuluma na mateso kutoka kwa utawala wa Korea Kaskazini. Rupert Colville ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.

“Hali ya watu wanaorudishwa kwa lazima nchini Korea Kaskazini imekuwa ikitia wasiwasi kwa miaka mingi. Wanaweza kuchukuliwa hatua kali  kwa kuihama nchi. Tunaamini kuwa wako kwenye hatari ya kukabiliwa na adabu kali wanaporudi nchini humo. Tumesikitishwa kuwa serikali za Laos na China zinaonekana kukiuka majukumu yao na hali waliyo watoto  wote wanaoripotiwa kuwa mayatima. Tunatoa wito kwa utawala nchini China na Laos kutangaza wazi hatma ya watoto hao tisa raia wa Korea Kaskazini  na  jinsi walivyorejeshwa kwao na kuiomba serikali ya Korea Kaskazini kuyapa nafasi mashirika huru  kuthibitisha hali zao na kile walichofanyiwa.”

Mkuu wa haki za bindamau kwenye Umoja wa Mataifa anasema kuwa hata kama taifa la Laos si mwanachama wa mkataba kuhusu wakimbizi  ilikuwa na jukumu la kuwalinda watu ambao maisha yao yanaweza kuwa hataraini wanaporudi nchini mwao.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter