Papua New Guinea kurejelea hukumu ya kifo:

31 Mei 2013

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa inasema imesikitishwa na hatua iliyochukuliwa na serikali ya Papua New Guinea ya kuelekea kurejea hukumu ya kifo. Taifa hilo linataka kurejea hukumu ya kifo baada ya kufanyia marekebisho sheria zake za uhalifu hatua iliyopitishwa na bunge Mai 28.

Mabadiliko hayo ya Katiba yanatoa njia tano za unyongaji na utekelezaji wa hukumu ya kifo kwa makosa mengine matatu ambayo ni mauaji yanayohusiana na ushirikina, ubakaji na unyang’anyi wa kutumia nguvu.

Papua New Guinea imesitisha hukumu hiyo kwa muda mrefu tangu mwaka 1954 na kasha kupitishwa kuwa sheria mwaka 1970. Ofisi ya haki za binadamu inasema wakati dunia sasa inajitahidi kufuta hukumu ya kifo hatua ya kurejelea hukumu hiyo ni kurudi nyuma. Na imeitaka serikali ya nchi hiyo kwa mara yingine kuzingatia sheria zake na kuungana na nchi nyingine duniani kuachana na hukumu ya kifo.