Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutowatenga watoto walemavu kunafaidisha jamii nzima: UNICEF

Kutowatenga watoto walemavu kunafaidisha jamii nzima: UNICEF

Shirika la Kuhudumia Watoto katika Umoja wa Mataifa, UNICEF, limesema watoto wengi na vijana wenye ulemavu bado hukumbana na aina nyingi za ubaguzi na kutengwa, na hivyo kunyimwa fursa ya kuishi kikamilifu na kuchangia maendeleo ya kijamii, kitamaduni na kiuchumi mahali wanakoishi. George Njogopa na taarifa kamili. (TAARIFA YA GEORGE)

Katika taarifa yake ya kila mwaka juu ya hali ya ustawi wa watoto UNICEF imesema kuwa watoto wanakabiliwa na hali ya ulemavu wanakabiliwa na mazingira magumu ya kufikiwa na hudumu muhimu ikiwemo matibabu na fursa ya kwenda shule.

Ama ripoti hiyo imebainisha kuwa watoto hao wanaandamwa na jinamizi jinginekamavile kukumbwa na vitendo vya unyanyasaji,mateso,kupuuzwa na kuachwa katika mazingira hatarishi.

Ripoti hiyo imesema kuwa watoto wenye ulemavu hawapaswi kutizamwakamachombo kinachosubiriwa kupatiwa hisani ya misaada, bali ni watoto wenye haki zote ikiwemo haki ya kuishi, huduma bora za afya, elimu na lishe.

Abid Aslam wa  UNICEF anasema kuwa ripoti ya mwaka huu inawahimiza watu kuwatizama watoto mbali na ulemavu.

 (SAUTI YA ASLAM)

Wanazo ndoto.Wanazo njia kutimiza ndoto hizo. Kama tulivyobainisha kwenye ripoti hii…wakipewa fursa wanao mchango mkubwa kwa familia zao na jamii kwa ujumla. Hii inamaanisha kwamba lazima kuchukuliwa hatua za kweli kuwasaidia watoto wenye ulemavu.Kuelewa mahitaji yao ikiwemo kuwajumuisha wao wakati kusaka majawabu ya shida zao ikiwemo pia wakati wa uandaaji wa tathmini ya huduma zinazowafaa ambazo zitawawezesha kuendelea kudumu, kung’ara na kufankiwa.