Wagombea wanawake Iran kupigwa marufuku kwatia hofu:UM

29 Mei 2013

Kundi la wataalamu huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa leo wameonya kwamba vikwazo visivyo vya lazima vilivyowekwa dhidi ya raia wa Iran kugombea nafasi ya urais, ubaguzi dhidi ya wagombea wanawake na masharti yanayoendelea dhidi ya uhuru wa kujieleza, kukusanyika na kukutana kwa amani ,ni ukiukaji mkubwa wa uhakikishaji wa haki za binadamu chini ya sheria za kimataifa.Wataalamu hao wanasema Mei 21 baraza la walezi lenye wajumbe 12 ambalo hupitisha majina ya wagombea wa Urais lilipitisha majina 8 tuu kati ya majina 686 ya watu walioajiandikisha kama wagombea  kwa ajili ya uchaguzi wa Urais uliopangwa kufanyika Juni 14.

Wanasiasa mashuhuri na wagombea wote 30 wanawake walikataliwa jambo ambalo limazusha hofu kuhusu usawa na uwazi wa mchakato mzima wa uchaguzi.

Wameongeza kuwa wengi wa wagombea walikataliwa tuu kwa sababu ya ushiriki wao kwenye maandamano ya baada ya uchaguzi wa 2009 na kutekeleza haki zao za msingi ikiwemo uhuru wa kujieleza, kukusanyika na kukutana.

Kamala Chandrakirana ambaye hivi sasa anaongoza kitengo cha Umoja wa Mataifa cha kupinga ubaguzi dhidi ya wanawake anasema kutowashirikisha wanawake kwenye uwezo wa kushika nafasi za juu za maamuzi ya kisiasa ni ubaguzi na ni kinyume na misingi ya kimataifa inayosema watu wasibaguliwe kutokana na jinsia.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud