FAO yapendekeza mtindo wa ukulima endelevu ili kukidhi mahitaji ya chakula

28 Mei 2013

Shirika la Chakula na Kilimo, FAO linapigia debe mtindo wa ukulima unaojali mazingira uitwao Hifadhi na Kukuza, na ambao linasema una uwezo wa kuongeza uzalishaji wa mihogo kwa hadi asilimia 400, na kuufanya mumea unaochukuliwa kama chakula cha watu maskini kuwa mumea wa karne ya 21. Joshua Mmali na taarifa kamili(RIPOTI YA JOSHUA MMALI)

Katika chapisho lake jipya la mwongozo kuhusu upandaji wa mihogo kwa viwango vidogovidogo, shirika la FAO limesema uzalishaji wa mihogo kote duniani umeongezeka kwa asilimia 60 tangu mwaka 2000, na unatarajiwa kuongezeka hata kwa kasi zaidi katika mwongo huu wakati watunga sera wanapotambua umuhimu mkubwa wa zao hilo.

Hata hivyo, matumizi ya virutubishaji vilivyoanzishwa katika karne ilopita ili kuongeza uzalishaji wa mihogo yana hatari ya kuharibu uhimili asilia wa mumea huo na kuongeza kuvuka kwa gesi chafuzi zinazochangia mabadiliko ya tabianchi.

Shirika la FAO linasema, suluhu ni kutumia mtindo wa Hifadhi na Kukuza, ambao unaongeza mazao kwa kuboresha udongo badala ya kutumia kemikali nyingi katika uzalishaji. Mtindo wa Hifadhi na Kukuza unapunguza uharibifu wa mchanga unaosababishwa na kulima, na unapendekeza kinga ya udongo kwa kuchanganya mimea shambani.