Maliasili ya Afrika inaweza kuchochea mabadiliko ya kiuchumi:UM

28 Mei 2013

Afrika lazima ijikite na kuimarisha kilimo chake, uchimbaji madini na rasilimali za nishati ili kukuza uchumi wake, imesema ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa na washirika wake iliyotolewa Jumatatu nchini Morocco.

Ripoti hiyo ambayo ni “Mtazamo wa kiuchumi wa Afrika 2013” inasema kwamba nchi za Afrika lazima zitumie utajiri wa rasili mali zake ili kuchagiza ukuaji wa uchumi na kuhakikisha kwamba mchakato hup unawanufaisha Waafrika wa kawaida.

Pia imesisitiza kwamba mchakato huo lazima ujumuishe sera za kijamii ambazo zinapunguza kpengo la kutokuwepo usawa katika bara hilo.

Kwa mujibu wa waandishi wa ripoti hiyo sasa ndio wakati muafaka wa kuanza kufanya mabadiliko ili uchumi barani Afrika uweze kuwa katika soko la ushindani na pia kutoa fursa za ajira kwa watu wake.

Ripoti inasema matarajio ya uchumi barani Afrika kwa 2013 na 2014 yanatia matumaini huku uchumi ukitarajiwa kukua kwa asilimia 4.8 mwaka huu na asilimia 5.3 mwaka ujao.

Hata hivyo ripoti imesisitiza kwamba ukuaji uchumi pekee hautotosheleza kupunguza umasikini, kukabili tatizo la ajira, kushughulikia kutokuwepo usawa wa kipato na kuporomoka kwa kiwango cha afya na elimu.