Viongozi wa Ukanda wa Maziwa Makuu walaani vurugu Mashariki mwa DRC

27 Mei 2013

Mkutano wa kwanza wa kikanda wa usimamizi wa amani, usalama na ushirikiano katika Jamhuri ya kidemokrasia yaCongo, DRC na ukanda wa maziwa makuu umemalizika hukoAddis Ababa,Ethiopiaambapo taarifa ya pamoja iliyotolewa mwishoni mwa kikao hicho pamoja na mambo mengine imelaani vurugu zinazoendelea huko Mashariki mwa DRC.  Taarifa hiyo imesema viongozi wanatambua uwepo wa vikundi vinavyosababisha vurugu kwenye eneo hilo na kwamba wanaunga mkono hatua za jumuiya ya kimataifa za kudhibiti vitendo hivyo ikiwa ni pamoja na kupelekwa kwa brigedi ya kujibu mashambulizi itakayokuwa chini ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani huko DRC, MONUSCO. Viongozi wa nchi hizo kumi ikiwemo Zambia, Uganda, Tanzania, Sudan Kusini, Afrika Kusini, Rwanda, DRC, Burundi na Angola wamesema pia wanaunga mkono mpango wa mashauriano baina ya pande husika ambao utawezesha kufanikiwa kwa mpango wa amani uliotiwa saini huko Addis Ababa mwezi Februari. Wamepongeza jitihada za mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye maziwa makuu, Mary Robinson na vile ambavyo anafanya mashauriano na serikali ya DRC, serikali za kitaifa, jumuiya za kikanda na za kimataifa. Taarifa hiyo imewakariri viongozi hao wakiwasihi wahisani kujitolea kwa rasilimali ili kuwezesha maendeleo ya ukanda wa maziwa makuu.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter