Umwagaji damu nchini Syria haukubaliki; mjadala wa dharura kufanyika Jumatano Geneva.

27 Mei 2013

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema jumuiya ya kimataifa inashindwa kutimiza wajibu wake kwa wahanga wa mzozo waSyriakwa kuruhusu vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini humo kuendelea bila wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria. Kamishna Mkuu wa haki za binadamu Navi Pillay amesema hayo wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva, Uswisi siku ya Jumatatu na kusema kuwa ukiukwaji huo wa haki za binadamu ni sawa na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu ambao hauwezi kuachiwa kuendelea bila hatua kuchukuliwa. Bi. Pillay amesema vikosi pinzani na serikali vinatumia raia kama ngaoyao katika mapigano ilhali serikali yaSyria inaendelea kutumia nguvu kupita kiasi na kushambulia bila kuchagua hata kwenye makazi ya raia, pamoja na shule na hata hospitali. Amesema umwagaji damu na mateso yanyokumba wananchi waSyria yamekuwa hayavumiliki mbele ya binadamu.

(SAUTI YA PILLAY)

 "Matukio yanahusisha madai kuwa baadhi ya vikundi vya upinzani vimelazimisha wasichana na watoto wadogo wa kike kuolewa na wapiganaji. Na tunaendelea kuona ripoti wapiganaji wa upinzani wakifanya vitendo katili vya kihalifu kama vile mateso na hata mauaji. Nina wasiwasi mkubwa kutokana na ripoti za sasa kuwa mamia ya raia wameuawa au kujeruhiwa na melfu wanaweza kuwa wamenaswa kwenye mashambulizi ya makombora na yale ya angani yanayofanywa na majeshi ya serikali huko Al Qusayr. Raia wanapaswa kupatiwa njia salama ya kupita ili kujiokoa, kwa mara nyingine tena nalazimika kulisihi baraza la uaslama kuwasilisha katika mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai, ICC. Tunapaswa kuweka bayana kwa serikali na wapinzani kuwa kutakuwepo na kuwajibika kwa vitendo vyao vya sasa.

Katika hatua nyingine Baraza la haki za binadamu litakuwa na mjadala wa dharura kuhusu hali ya binadamu Syria siku ya Jumatano licha ya upinzani mkali kutoka serikali za Syria, Cuba na Venezuela. Mjadala huo unafuatia ombi la pamoja lililowasilishwa Ijumaa iliyopita na Marekani, Qatar na Uturuki.