Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama latambua mchango wa mahakama ya ICTY

Baraza la usalama latambua mchango wa mahakama ya ICTY

Wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa Jumamosi wameadhimisha mwaka wa 20 tangu kuundwa kwa mahakama ya uhalifu kufuatia vita vya Balkan katika miaka ya 1990.

Katika taarifa yake maalumu baraza limesema linakumbuka azimio nambari 827 la tarehe 25 Mai mwaka 1993 ambalo lilipitishwa bila kupingwa na wajumbe wote kuanzisha mahakama ya uhalifu dhidi ya Yugoslavia ya zamani (ICTY)

Baraza linasema kwa miaka yote hiyo linatambua mchango wa ICTY katika vita dhidi ya ukwepaji mkono wa sheria hasa kwa uhalifu mkubwa unaoigusa jumuiya ya kimataifa.

Wajumbe pia wamekaribisha kuanza hapo Julai mosi kwa tawi la mfumo wa kimataifa wa mahakama za uhalifu litakalokuwa na makao The Hague na kusisitiza kwamba tawi hilo ni muhimu ili kuhakikisha kwamba kufungwa kwa mahakama ya uhalivu ya Rwanda ICTR na mahakama ya ICTY hakutafungua mlango wa wahalifu ambao bado wanatafutwa kukwepa mkono wa sheria.

Na baraza limerea kusisitiza kwamba litahakikisha vita dhidi ya ukwepaji mkono wa sheria vinaendelea na hakuna atakayepata fursa ya kufanya hivyo.  Tangu kuanzishwa mahakama ya ICTY imeshawatia hatiani watu 161.