Mkuu wa UNESCO amuenzi mwanamuziki Georges Moustaki

24 Mei 2013

Mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO ameelezea simanzi aliyonayo kufuatia taarifa za kifo cha mwanamuziki Georges Moustaki.Mwanamuziki huyo ambayo ni mtunzi na muimbaji  alikuwa ni maarufu na nembo ya muziki wa Urafansa na msanii wa amani wa UNESCO.

Alifariki dunia Alhamisi Mai 23. Kufuatia kifo hicho Bokova amesema dunia imepoteza mshahiri mahiri na msanii aliyekuwa na hadhi ya kimataifa.

Moustaki aliandika miongoni mwa nyimbo bora na nzuri saana zilizoimbwa na wasanii wengine mbalimbali wakiwemo,Barbara Juliet Greco, Serge Reggiani, Edith Piaf na Yves Montand. Alizaliwa mwaka 1934 nchini Misri na wazazi Wagiriki. Alitambulika rasmi kimuziki mwaka 1969 alipotoa kibao Le Meteque kibao kilichomuingiza katika ramani ya kimataifa kimuziki.

Na tarehe 14 Sept 1999 alitangazwa na UNESCO kuwa msanii wa amani wa shirika hilo hasa kwa mchango wake wa kupigia upatu  utamaduni wa amani na kuunga mkono malengo ya UNESCO.Kwa niaba ya UNESCO Bokova ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Moustaki, marafiki na wasanii wa muziki waliomfahamu kote duniani.