Reinada Milanzi: Mlinzi wa amani kutoka Tanzania aliyejikita kujenga uhusiano wa kijinsia katika jamii

24 Mei 2013

Shughuli za ulinzi wa amani ni zaidi ya kuzuia mapigano bali pia kuweka mazingira ambamo kwao uhusiano wa kijamii unaweza kuwa bora na maisha yakasonga mbele, kwani chokochoko za kijamii zinaweza kuwa chanzo cha mapigano ya kivita. Mathalani ukatili wa kingono na unyanyasaji wa kijinsia unaweza kukithiri katika maeneo ya migogoro lakini pindi amani inapopatikana basi suala hilo nalo lazima lishughulikiwe ili mchakato wa amani usonge mbele.

Umoja wa Mataifa kupitia walinzi wa amani hutekeleza majukumu hayo ili wale waliokumbwa na ukatili huo waone sheria inachukua mkondo wake. Hilo ni moja ya majukumu aliyofanya Reinada Milanzi, Afisa Polisi kutoka Tanzania akihudumu na kikosi cha pamoja cha Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika huko Darfur, UNAMID kati ya Machi 2010 hadi Machi 2013. Hapa katika mahojiano na Assumpta Massoi wa Idhaa hii, alizungumzia changamoto alizokumbana nazo na kile alichofurahia zaidi. Lakini kwanza anaanza kwa kueleza alivyopokea wito wa kwenda Darfur.