Wanawake na watoto wana haki ya kuishi kwa usalama na heshima: Ban

23 Mei 2013

Wanawake na watoto wana haki ya kuhisi wako salama na kuishi kwa utu, popote pale na wakati wote, iwe katika vita na amani, umaskini na utajiri, nyumbani na nje, shuleni na katika sehemu za kazi.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ambaye yupo mjini Kigali Rwanda, wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi wa kituo cha kupiga vita ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Kituo hicho ni miongoni mwa vituo ambavyo vimewekwa nchini humo, ambako wahanga na manusura wa wanaweza kupata usaidizi wa bure kisheria, kiafya na ushauri nasaha. Bwana Ban amesema kituo hicho kitaongeza ushirikiano baina ya taasisi za kisheria kote barani Afrika.

Bwana Ban ameisifu Rwanda kwa kujitolea kwake kisiasa kuzuia na kupiga vita dhuluma dhidi ya wanawake na watoto, na kwa kuongoza kuchangia polisi wa kike kwenye vikosi vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa.

Bwana Ban amesema, wakati msingi wa kituo hicho ukiwekwa, ni vyema kutambua kuwa wanawake na wasichana ndio msingi wa jamii zote, na kutoa wito kwa wote kuungana ili kubadili desturi na dhana zinazochochea, kuendeleza na hata kuruhusu ukatili dhidi ya wanawake.