Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano yasababishwayo na M23 Mashariki mwa DRC yanatia wasiwasi: Ban

Mapigano yasababishwayo na M23 Mashariki mwa DRC yanatia wasiwasi: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon anaendelea na ziara yake ya Ukanda wa Maziwa Makuu barani Afrika ambapo leo yukoRwanda na kubwa ni kuchagiza mchakato wa kuleta amani huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, DRC. Kabla ya kuelekea Rwanda Bwana Ban alizungumza na Radio Okapi huko DRC na kuelezea wasiwasi wake juu ya mwendelezo wa mapigano Mashariki mwa nchi hiyo.(SAUTI BAN)

Hali ni tete. Hali hiyo haiwezi kupuuzwa. Nina wasiwasi mkubwa na kuendelea kuibuka kwa mapigano mara kwa mara yanayosababishwa na M23 na ni matumaini yangu ya dhati kuwa pande zote husika hususan FARDC na M23 na pande zingine zitatatua hali hii kwa mazungumzo. Mashauriano ya Kampala ni lazime yaanze tena ili kumaliza mapigano haya.”

 Na taarifa zaidi kuhusu mapigano hayo huyu hapa George Njogopa.

(RIPOTI YA GEORGE NJOGOPA)

 Mapigano mapya yalizuka hapo siku ya jumanne baina ya vikosi vya serikali na kundi la waasi la M23 yalivuruga ustawi wa eneo la jimbo la Kivu Kaskazini.  Mara ya mwisho pande hizo mbili kushambuliana ilikuwa April mwaka uliopita 2012 na tangu wakati huu kumekuwa na wimbi kubwa la raia waliokwenda mtawanyikoni kwa hofu ya mapigano hayo.

Kiasi cha watu wanaokadiriwa kufikia 60,000 wameripotiwa kukimbilia katika nchi jirani zaUgandanaRwandakwa ajili ya kuomba hifadhi.

Katika taarifa yake kuhusiana na mapigano hayo ya hapo majuzi,shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema kuwa limeingiwa na hofu kuhusiana na usalama wa raia walioko kwenye makambi za  mjini Goma.

Shirika hilo la wakimbizi limezitolea mwito pande zote kuchukua jukumu la kuwalinda raia ikiwemo wale waliokosa makazi.