Fistula yatibika, kila mmoja aahidi kuizuia: UNFPA

22 Mei 2013

Mvua inanyesha lakini hali hii haikumzuia Essita Mulhanga, msichana wa umri wa miaka Kumi na Sita kuweza kujikongoja hadi hospitali ili aweze kupata tiba…..Ana maumivu makali na punde tu baada ya kufika hapa akaeleza.. 

SOUNDBITE (Shona) Essita Mulhanga, 16-anayeumua fistula:

"Nililazimika kujifungulia nyumbani. Mume wangu hakuwepo kunisaidia. Baada ya kujifungua, nilichanika vibaya, tatizo hili likanianza nashindwa kuzuia haja ndogo.”

Essita si pekee katika machungu haya yajulikanayo kama Fistula. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa wanawake na wasichana kati ya Milioni Mbili na Tatu katika nchi zinazoendelea wanaugua Fistula.

Fistula ni hali itokanayo na uchungu wa uzazi wa muda mrefu unaosababisha tundu katika sehemu za siri. Na hali inatisha zaidi kwani kila mwaka kuna wagonjwa wapya Elfu Hamsini. Na kutokana na harufu kali ya kuchanganyika kwa haja ndogo na haja kubwa, wanawake walio na hali hiyo huonekana ni wachafu na mara nyingi hukabiliwa na unyanyapaa mkuwba kwenye jamii zao.

Fistula imeweza kutokomezwa nchi tajiri. Kwa sasa janga ni kwa nchi maskini na mara nyingi ni vigumu wagonjwa kufikiwa. Hili ni jambo ambalo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la idadi ya watu duniani, UNFPA, Dkt. Babatunde Osotimehin, anasema ni zaidi ya upatikanaji wa huduma za afya.

(SAUTI:Dr. Babatunde Osotimehin)

"Hii haikubaliki katika dunia ya leo. Inaonyesha pia, kwa maoni yangu kuwa thamani ya wanawake katika jamii zetu na ukweli kwamba hatuwekezi vya kutosha kwa watoto wetu wa kike na wanawake.”

Kampeni ya kutokomeza fistula ilianzishwa na UNFPA miaka kumi iliyopita ili kuepusha wanawake na watoto wa kike dhidi ya hali hiyo na wale waliokwisha kukumbana nayo waweze kupatiwa tiba. Na kesho tarehe 23 mwezi Mei ni maadhimisho ya kwanza ya siku ya kutokomeza Fistula duniani. Mtendaji mkuu wa UNFPA anaamini siku kama ya kesho itachochea zaidi harakati dhidi ya Fistula.

(SAUTI:Dr. Babatunde Osotimehin)

"UNFPA inapenda kila anayesikia ujumbe huu au atakayeshiriki maadhimisho ya kwanza ya kutokomeza Fistula duniani yeye mwenyewe aahidi kutokomeza hali hiyo kwenye jamii yake. Iwapo tutafanya hivyo, tunaweza kuhakikisha kuwa kila mjamzito anapata huduma stahili na sahihi pindi anapohitaji. Na hicho ndicho tunahitaji ili kutokomeza Fistula.”

UNFPA inasema kuwa wakati upasuaji maalum unahitajika kurekebisha mwanamke aliyechanika au mwenye Fistula, wakati mwingine yahitajika zaidi ya upasuaji mmoja kama ilivyokuwa kwa Essita ambaye atahitaji tena operesheni nyingine ili awe na matumaini zaidi kwa maisha yake.

(SAUTI:Shona) Essita Mulhanga)

"Baada ya tiba, ningependa kuwa na watoto, na ningependa nione wanasoma na kuwa madaktari au walimu.”

Mpaka sasa UNFPA imesaidia zaidi ya wanawake na watoto wa kike elfu thelathini na wanne kupata upasuaji ili kutibu Fistula.