Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bi Robinson ahofia kuzuka tena mapigano mashariki mwa DRC

Bi Robinson ahofia kuzuka tena mapigano mashariki mwa DRC

Mwakilishi wa Katibu Mkuu katika nchi za ukanda wa Maziwa Makuu, Mary Robinson, ameelezea wasiwasi wake kufuatia kuzuka tena kwa mapigano hivi karibuni katika maeneo karibu na mji wa Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, DRC, akitolea wito uungwaji mkono wa juhudi zote zinazoendelea ili kuleta amani na utulivu katika ukanda huo.

Bi Ribinson amesema kuteseka na kulazimika kwa watu kuhama mashariki mwa DRC, hususan wanawake na watoto, kumeendelea kwa muda mrefu sana, na hakuwezi kukubalika kuendelea zaidi.

Bi Robinson ameitoa kauli hii wakati akitoa mapendekezo ya kanuni zitakazotumiwa kuongoza juhudi za sasa za kuutatua mzozo wa ukanda huo, huku akisisitiza uzingatiwe mtazamo wa suluhu la kudumu.

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa pia ametoa wito hatua zichukuliwe kuongeza kasi ya urejeaji nyumbani wakimbizi kwa hiari, na kuzindua tena programu za kuyavunja makundi yenye silaha.

Bi Robinson ataungana na Katibu Mkuu Ban Ki-moon na rais wa Benki ya Dunia Jim Yong Kim katika ziara yao nchini DRC kuanzia tarehe 22 hadi 24 Mei.