Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huduma ya afya kwa wote ni msingi wa kutokomeza umaskini: Benki ya Dunia

Huduma ya afya kwa wote ni msingi wa kutokomeza umaskini: Benki ya Dunia

Benki ya dunia imetaka jitihada za kimataifa zichukuliwa katika kuhakikisha kila mtu duniani ana uwezo wa kupata huduma bora za afya. Akihutubia kikao cha mwaka cha baraza kuu la shirika la afya duniani, WHO huko Geneva, Uswisi, Rais wa Benki ya Dunia, Jim Yong Kim amesema ili kufikia lengo la kutokomeza ufukara mwaka 2030, nchi zote zinapaswa kuhakikisha raia wake wana uwezo wa kupata huduma bora za afya. Amesema wakati nchi hizo zitahigaji uchumi bora na jumuishi ili kuondoa umaksini, halikadhalika zinapaswa kuwekeza katika kuboresha afya, elimu, na hifadhi ya jamii kwa raia wote.

 (SAUTI- KIM)

 “Kwa makadirio ya sasa, gharama za afya zinatumbukiza watu Milioni 100 katika umaskini wa kupindukia kila mwaka na kuwasababishia wengine Milioni 150 mazingira magumu ya kifedha. Hii ni aina mbaya ya ugumu wa maisha kwa watu kwa kuwa machungu ya umaskini yanachanganyika na magonjwa. Kupanua utoaji wa huduma ya afya miongoni mwa maskini kwenye nchi yoyote ile ni muhimu katika kujenga uwezo na kuwawezesha kuingia katika ushindani wa ajira ambao utabadili maisha yao. Tunapaswa kuondoa hili pengo la huduma za afya iwapo tuko makini katika kuondoa tofauti za kiuchumi, kuimarisha nchi zetu kiuchumi na kujenga jamii ambazo kwazo kila mtu ana fursa sawa.”

 Bwana Kim amesema Benki ya dunia iko makini kusaidia nchi kufikia malengo ya maendeleo ya mileni kwa kupunguza vifo vya wajawazito na watoto akieleza kuwa huo ni mtihani mkuu kwa ahadi ya benki hiyo ya kuweka uwiano wa afya.