Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Changamoto za kiuchumi zazorotesha usalama wa chakula na hali ya lishe Misri: WFP

Changamoto za kiuchumi zazorotesha usalama wa chakula na hali ya lishe Misri: WFP

Ripoti mpya iliyotolewa Jumanne inaonyesha kuzidi kuongezeka kwa umaskini na ukosefu wa uhakika wa chakula nchini Misri kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Grace Kaneiya ana ripoti zaidi.

(SAUTI YA GRACE)

Ripoti hiyo iliyoandaliwa kwa ushirika kati ya shirika la mpango wa chakula duniani WFP, taasisi ya kimatifa ya utafiti wa sera za chakula na taasisi kuu ya takwimu za umma nchini Misri inaonyesha kuwa asilimia 17 ya wamisri wote hawakuwa na uhakika wa chakula mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 14 mwaka 2009.

Halikadhalika kiwango cha utapiamlo unaonekana miongoni mwa watoto waliodumaa wenye umri wa chini ya miaka mitano kinaongezeka. Mwakilishi mkazi wa WFP nchini Misri, GianPetro Bordignon amesema ukosefu wa uhakika wa chakula siyo kitu kilichoibuka tu mara moja bali ni matokeo ya majanga yaliyopokezana tangu mwaka 2005.

Majanga hayo ni pamoja na mlipuko wa homa ya mafua ya ndege na kupaa kwa bei za vyakula na mafuta. Ripoti hiyo imesema ruzuku ya chakula imekuwa na msaada mkubwa kwa maskini lakini haijaweza kumaliza chanzo cha umaskini.

Badala yake ripoti imependekeza mambo kadhaa ikiwemo kuanzishwa kwa fursa za ajira katika maeneo ya maskini.