Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO yaingiwa wasiwasi na mapigano mapya huko Goma

MONUSCO yaingiwa wasiwasi na mapigano mapya huko Goma

Kumeripotiwa kuzuka upya kwa mapigano kwenye eneo la Kibati na Rusayo huko Goma mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, DRC, alfajiri ya Jumatatu kati ya vikosi vya serikali na waasi wa kundi la M23 ambapo Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO umeelezea wasiwasi mkubwa.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Eduardo de Buey amewaambia waandishi wa habari mjini New York, Marekani kuwa mapigano hayo kilometa 12 kutoka Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini yamehusisha matumizi ya silaha nzito, maroketi na makombora ambapo jeshi la DRC limeripotiwa kutumia helikopta katika moja ya operesheni zake.

Del Buey amesema MONUSCO ina wasiwasi juu ya tukio hilo na kwamba ujumbe huo unafuatilia harakati za kisiasa na kidiplomasia za kudhibiti na kumaliza mapigano hayo kati ya serikali na waasi wa M23.

Ripoti hizi za mapigano mapya zinakuja wiki chache tangu Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye Maziwa Makuu, Mary Robinson aripoti kuwepo kwa dalili za kutia moyo za kusukuma mbele mchakato wa amani huko DRC.