Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban na Putin wajadili Syria, Afghanistan na Mashariki ya Kati

Ban na Putin wajadili Syria, Afghanistan na Mashariki ya Kati

Naunga mkono makubaliano kati ya Urusi na Marekani ya kuandaa kongamano la kimataifa kuhusu Syria, na hiyo ni moja ya kauli za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon alizotoa wakati wa mazungumzo yake na Rais Vladmir Putin wa Urusi huko Sochi hii leo. Bwana Ban amesema kongamano hilo litasaidia pande husika huko Syria kuanza kutekeleza makubaliano ya Geneva ya tarehe 30 Juni 2012 ya kuanzisha chombo tendaji cha mpito chenye mamlaka kamili. Wamejadili pia umuhimu wa kuungwa mkono kwa kongamano hilo na kanda husika sambamba majukumu ya mjumbe wa pamoja wa  Umoja wa Mataifa na nchi za kiarabu kwenye mzozo wa Syria, Lakhdar Brahimi. Bwana Ban na Rais Putin pia walizungumzia masuala ya Mashariki ya Kati, Afghanistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea na mabadiliko ya Tabia nchi ambapo pia Katibu Mkuu ametoa shukrani kwa jinsi Urusi inaunga mkono masuala ya ulinzi wa amani.