Ban ajadili suala la Syria na viongozi wa Urusi huko Sochi

17 Mei 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov wameafikiana kwamba mkutano wa kimataifa kuhusu Syria ufanyike haraka iwezekanavyo ili kuzisaidia pande husika katika machafuko kufanya majadiliano.

Joshua Mmali na taarifa kamili

Suluhu litokanalo na mazungumzo ya kisiasa ndiyo njia pekee itakayoumaliza mzozo wa Syria, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon.

Bwana Ban amesema hayo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Sochi, Urusi, ambao pia ulihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov.

Ameongeza kuwa changamoto kubwa sasa ni kuitumia kasi ya msingi ulowekwa na Waziri Lavrov wa Urusi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, na kuwashukuru hao wawili kwa uongozi wao.

Bwana Ban na Waziri Lavrov pia wamejadili jinsi gani mgogoro huo wa Syria unavyoathiri ukanda mzima wa Mashariki ya Kati.

(SAUTI YA BAN KI-MOON)

Wakati Katibu Mkuu akisema hivyo, Shirika la Kuhudumia Wakimbizi katika Umoja wa Mataifa, UNHCR, limesema idadi ya watu walokimbilia nje ya Syria sasa imezidi milioni 1.5, huku ufadhili kwa ajili ya misaada wanayohitaji wakimbizi hao ukiwa bado ni haba. Na habari za hivi punde zinasema tayari Bwana Ban amekuwa na mazungumzo na Rais Vladmir Putin wa Urusi.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter