Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita dhidi ya Pepo punda yaweka historia: UNICEF

Vita dhidi ya Pepo punda yaweka historia: UNICEF

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema hatua ya kihistoria imefikiwa katika kutokomeza ugonjwa wa Pepopunda miongoni mwa mama na watoto wachanga ambapo zaidi ya nusu ya nchi 59 zilizokuwa na ugonjwa huo zimeweza kuutokomeza.

Taarifa ya UNICEF inesema kuwa Pepopunda ambayo husababisha kifo cha mtoto mmoja mchanga katika kila dakika Tisa, ni ugonjwa unaozuilika kwa chanjo anayopatiwa mama mjamzito. Hata hivyo imesema ugonjwa huo huambukizwa kwa mtoto mchanga pindi anapozaliwa katika mazingira machafu, na vifaa visivyotakatishwa kutumiwa kukata kitovu.

Miongoni mwa nchi zilizotokomeza ugonjwa huo ni pamoja na Burundi, China, Msumbiji, Malawi, Uganda na Tanzania, huku Kenya, Somalia na Angola zikiwa miongoni mwa nchi zilizo kwenye hatua za mwisho za kutokomeza ugonjwa huo.

UNICEF inasema tangu mwaka 1999, zaidi ya wanawake Milioni 118 kwenye nchi 52 walio na umri wa kuzaa watoto wamechanjwa dhidi ya Pepopunda.