Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza Kuu la UM lapitisha azimio kuhusu Syria

Baraza Kuu la UM lapitisha azimio kuhusu Syria

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio ambalo pamoja na mambo mengine linatoa wito wa kuharakishwa mchakato wa mpito wa kisiasa nchini Syria huku likieleza masikitiko yake kutokana na ongezeko la idadi ya vifo kila uchwao nchini humo.

Upigaji kura ulionyesha nchi 107 zikiunga mkono, nchi 12 zikipinga huku nyingine 59 zikijiepusha kuonyesha msimamo wowote. Azimio hilo lililowasilishwa na nchi za kiarabu linashutumu vikali serikali ya Syria kwa matumizi ya silaha nzito kwenye mzozo huo na kuenea kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na kukandamizwa kwa uhuru wa kimsingi.

Nchi zilizopinga azimio hilo ni pamoja na Syria yenyewe ambapo Mwakilishi wake wa Kudumu katika Umoaj wa Mataifa Balozi Bashar Ja’Afari akizungumza kabla ya upigaji kura alisema kuwa maudhui ya azimio hilo yanakinzana na lengo la azimio akisema kuwa yanalenga kuhalalisha upatiaji silaha wale aliowaita magaidi nchini Syria.

Hata hivyo Rais wa Baraza Kuu Vuk Jeremic alisema ghasia nchini Syria zinazidi, halikadhalika chuki na akahoji iwapo watashindwa kusitisha mgogoro huo wanaweza kuendeleza uhalali wa kimaadili wa Umoja wa mataifa.

Hili ni azimio la Tano juu ya Syria kupitishwa na Baraza Kuu tangu mwaka 2011 pindi mapigano yalipozuka katika ya serikali na vikosi vya upinzani.