Hali Eritrea ifuatiliwe kwa karibu: Mtaalam wa UM

14 Mei 2013

Mtaalam maalum mpya wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Eritrea, Sheila B. Keetharuth, ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kufuatilia kwa karibu sana hali nchini Eritrea hadi hapo mabadiliko kamili yatakapodhihirika nchini humo.

Mtaalam huyo ambaye amekamilisha ziara ya siku kumi nchini Ethiopia na Djibouti, ilokusudiwa kukusanya maelezo kutoka kwa wakimbizi wa Eritrea kuhusu hali ya haki za binadamu nchini mwao, amesema ukiukaji wa haki za binadamu bila kujali nchini Eritrea haiwezi kukubalika.

Bi. Keetharut amesema mabadiliko kamili nchini humo yatahitaji harakati za kina za marekebisho ambayo yataibadilisha desturi iliyopo sasa ya kukana ukiukaji wa haki za binadamu kuwa desturi ya uongozi wa kisheria, pamoja na kuheshimu haki zote za binadamu na utu wa mwanadamu.

Mtaalam huyo maalum ameonya kuwa idadi ya wakimbizi wengi wa Eritrea nchini Ethiopia na Djibouti ni ishara ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Eritrea, ambao unawalazimu watu kufanya uamuzi mgumu wa kuacha familia zao na kukimbilia maisha wasiyoyajua.