Ban afanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa CAR

14 Mei 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Nicolas Tiangaye, na kuelezea kuunga kwake mkono na kutambua uhalali wa mamlaka ya Waziri huyo mkuu, kutokana na makubaliano ya Libreville na azimio la N’Djamena.

Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wake, Bwana Ban amesisitiza kuwa kuwekwa kwa taasisi zinazoaminika na harakati zinazowajumuisha wote ni muhimu kwa ufanisi wa kipindi cha mpito.

Bwana Ban amerejelea ujumbe wake wa kusikitishwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaoendelea kote nchini, na hali ya kibinadamu inayozidi kuzorota. Amesema ni lazima ukiukwaji huo ukomeshwe na wanaoutekeleza kuwajibishwa kisheria.

Katika mkutano huo, wamejadili hali tete ya kiusalama inayoendelea nchini humo, na kuhimiza uongezwe uwezo wa kuwafikia watu wanaohitaji misaada.