Virusi vya polio isiyofahamika vyabainika Somalia, WHO yachunguza

14 Mei 2013

Uchunguzi umeanzishwa kuhusu ripoti ya kuwepo kwa virusi vivyojulikana aina ya WPV1 vya ugonjwa wa polio katika eneo la Banadir nchini Somalia.Shirika la afya duniani WHO linasema hivi ni virusi vya aina yake kuripotiwa nchini Somalia tangu mwezi Machi mwaka 2007 . Assumpta Massoi na taarifa kamili.

(RIPOTI YA ASSUMPTA MASSOI)

Virusi hivyo vilitenganishwa kutoka sampuli iliyochukuliwa tarehe 21 Aprili mwaka 2013 kwa mtoto wa kike mwenye umri wa miaka mitatu ambaye alidhoofika ghafla na kupooza tarehe 18 mwezi huo wa Aprili mwaka huu na pia sampuli zingine kutoka kwa watu watatu waliokuwa karibu naye.

WHO inasema kwa kuwa hakujatolewa chanjo kwenye sehemu nyingi za kati na kusini mwa Somalia tangu mwaka 2009 huenda virusi hivyo vikasambaa na kuwa na athari kubwa ya kiafya ndani na nje mwa Somalia.

Glen Thomas ni msemaji wa WHO

(SAUTI GLEN THOMAS)

“Leo WHO inaanza kampeni ya chanjo ya polio hadi tarehe 16 mwezi huu. Lengo ni kuwafikia watoto Laki Tatu na Elfu Hamsini walio na umri wa chini ya miaka mitatu katika wilaya zote 16 za jimbo la Banadir. Pamoja na chanjo tutafanya pia kampeni zingine za kitaifa za chanjo ambapo mjadala unaendelea.”