UNAMID yalaani mauaji Darfur

13 Mei 2013

Ujumbe wa Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa Darfur UNAMID unaungana na kiongozi wa pamoja wa Muungano huo Mohamed Chambas kulaani shambulio la kinyama la May 12 lililosababisha kifo cha Mohamed Bashar ambaye alikuwa kiongozi wa kundi la Justice and Equality Movement-Sudan (JEM/Bashar) na washirika wenzake.

Bwana Chambas amesema kundi hilo lilikuwa na nia thabiti katika utatuzi wa amani katika mgogoro huko Darfur pale lilipojiunga katika kusaini makubaliano ya amani ya Doha (DDPD) ya April 6 .

Akieleza rambirambi zake kwa familia za waliopoteza maisha Chambas amesema DDPD bado inanufaika na kuungwa mkono kutoka Muungano wa Afrika , Umoja wa Mataifa, na jumuiya ya kimataifa kwa ujumla ikiwa ni njia kuelekea amani ya kudumu.

Mwakilishi huyo maalum wa Umoja wa Mataifa amezitaka pande zote zinazozozana huko Darfur hususani vikundi vya kijeshi ambavyo havijatia saini makubaliano ya amani, kusitisha mapigano ,kuheshimu sheria ya kimataifa ya kibinadamu na kushiriki kikamilifu katika kurejesha amani kufuatia mgogoro.