Kutokomeza usafirishaji haramu wa watu kunahitaji uongozi wa kisheria: Ban

13 Mei 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon ametoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kusaidia katika kutokomeza usafirishaji haramu wa watu, na kujenga ulimwengu ambako mahitaji ya watu ya kimsingi yanatimizwa na haki zao kuheshimiwa.

Katibu Mkuu amesema mabilioni ya dola hutokana na usafirishaji haramu, unyanyasaji na kuwatumikisha vibaya watu, na fedha hizo hutumiwa kufadhili madawa ya kulevya, ufisadi na uhalifu mwingine.

Bwana Ban amesema, ili kutokomeza usafirishaji haramu wa watu na utumwa, ni lazima sauti za waathirika zisikilizwe, na wanaotenda uhalifu huo wawajibishwe kisheria.

(SAUTI YA BAN)

“Ili haki itendeke, tunahitaji msingi thabiti wa uongozi wa sheria. Hili linahitaji kutokomeza ufisadi ambao unafanyika katika biashara nyingi. Tunatakiwa kuimarisha mifumo ya sheria na kuzisaidia serikali kupata kuaminika na wananchi wao. Pia tunatakiwa kuendeleza viwango vya maisha. Usafirishaji haramu wa watu hunawiri katika mazingira ya umaskini. Watu hudanganywa kuondoka nyumbani kwao kwa ahadi za utajiri na usalama.”