Lolote lifanywe kutokomeza usafirishaji haramu wa watu: UM

13 Mei 2013

Kila juhudi zinapaswa kufanywa ili kutokomeza utumwa wa mamilioni ya watu, huku waathirika wakisaidiwa kuanza maisha mapya.  Hayo yamesemwa na rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataia, Vuk Jeremic, wakati wa mkutano wa Baraza hilo kuhusu mpango wa kimataifa wa hatua za kukabiliana na usafirishaji haramu wa watu.Bwana Jeremic amesema anaamini kuwa wakati hatua hizo zinapochukuliwa, waathirika wa usafirishaji haramu wa watu wanapaswa kuzingatiwa zaidi.

 (SAUTI YA JEREMIC)

“Ili kufikia lengo hili, maafisa wa sheria, maafisa wa mipaka, wakaguzi wa ajira, maafisa wa ubalozi, majaji, waendesha mashtaka, pamoja na walinda amani wanatakiwa, sio tu kuwa waangalifu zaidi, bali pia kueleweshwa kuhusu mahitaji ya waathirika. Wanatakiwa pia wafanye kazi kwa karibu sana na wahudumu wa kijamii watoaji misaada wengine. Tuwe kitu kimoja kwa suala hili, na kutokomeza jinamizi hili linaloivamia hadhi ya mwanadamu.”

Bwana Jeremic amesema, mkutano wa leo wa ngazi ya juu unatoa nafasi ya kutathmini ni nini kilichofanyika katika kujenga misingi minne ya mpango wa hatua za kuchukuliwa, ikiwemo kuzuia, kulinda, kuwajibisha wahalifu kisheria na ushirikiano, na kubuni njia za kuimarisha kazi ya ofisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu madawa ya kulevya na uhalifu.