Matarajio ya Guinea-Bissau mpya mwakani yapo licha ya changamoto: Ramos-Horta

9 Mei 2013

Mwakilishi maalum wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa huko Guinea-Bissau José Ramos-Horta amesema kuna dalili za matumaini nchini humo baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwaka jana ambapo tangu ashike wadhifa huo ameshirikiana na taasisi za kikanda ikiwemo Umoja wa Afrika na ECOWAS katika kuandaa mkakati wa pamoja wa kusaidia nchi hiyo kuharakisha mchakato wa sasa wa mpito ili uchaguzi ufanyike mwezi novemba.

Bwana Ramos-Horta amesema hayo katika mahojiano maalum na Radio ya Umoja wa Mataifa mjini New York ambapo amesema huo ndio ujumbe wake kwa baraza la usalama alipolihutubia hii leo kuhusu hali ilivyo nchini Guinea-Bissau.

(SAUTI-RAMOS)

“Ni lazima kuwe na serikali jumuishi, na hii inaweza kupatikana siku chache zijazo, au wiki moja au mbili ambayo itafungua njia kwa muungano wa Afrika kurejesha uanachama wa Guinea Bissau. Kwa sababu nchi za Afrika zimefanya jambo zuri, katika karne ya 21 huwezi kupanga kupindua serikali na kufikiri kwamba dunia itakuangalia tu na shughuli ziendelee kama kawaida. Tuna tumaini kwamba kutakuwa na Seriklai jumuishi hivi karibuni na uchaguzi Novemba kwa hiyo sio kwamba kila kitu ni kibaya”.

 Bwana Ramos-Horta amesema mashauriano anayaoongoza yana changamoto kwa kuwa wanasiasa mara kadhaa wanakuwa na hofu ya kupoteza madaraka kwani wakati mwingine mnayokubaliana, wanabadilisha kwa hiyo inapasa uvumilivu na kutopuuza jambo lolote.

Kuhusu biashara ya dawa za kulevya ameionya nchi hiyo iwe makini ichukue hatua kwani Marekani au nchi za Ulaya hazitokubali kuona wananchi wake wanaathirika kutokana na kupata madawa hayo yanayosafirishwa kupita upenyo wa Guinea Bissau.