Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Natumai kila mwenye haki ya kupiga kura Pakistani atafanya hivyo: Ban

Natumai kila mwenye haki ya kupiga kura Pakistani atafanya hivyo: Ban

“Nafuatilia kwa karibu maandalizi ya uchaguzi wa ngazi ya kitaifa na majimbo huko Pakistani na ni matumaini yangu kuwa kila raia mwenye haki ya kufanya hivyo ataweza kutekeleza haki yake hiyo ya kidemokrasia bila kujali dini, kabila wala jinsia.”

Hiyo ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon katika taarifa iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa hii leo akizungumzia uchaguzi huo wa tarehe 11 mwezi huu.

Bwana Ban amepongeza juhudi za serikali ya Paksitani na Tume ya uchaguzi, vyama vya siasa, viongozi wa kidini na mashirika ya kiraia kwa kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura hususan wanawake.

Hata hivyo ameonyesha wasiwasi wake juu ya ongezeko la matukio ya mashambulio nchini humo yanayolenga wanasiasa, waandamanaji na ofisi zinazohusika na masuala ya ucahguzi.

Ametuma rambi rambi kwa wahanga wa matukio hayo huku akisema anatambua juhudi za serikali ya Pakistani za kuhakikisha kuwa siku ya uchaguzi kunakuwepo na ulinzi na usalama kwa wagombea, wafanyakazi wa vyama vya siasa, maafisa na waangalizi wa uchaguzi.