UNESCO yalaani mauaji ya mwandishi-mtangazaji mkongwe huko Iraq

9 Mei 2013

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO limelaani kifo cha mwandishi na mtangazaji mkongwe wa radio huko Iraq kilichotokana na shambulio la bomu mjini Baghdad.  Kwa maelezo zaidi huyu hapa George Njogopa.

 (SAUTI YA GEORGE)

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Bi Bokova, amesema kuwa amevunjwa moyo na kusikitishwa kufuatia taarifa za kuuwawa kwa mwandishi huyo wa habari ambaye amemwelezea kama moja ya waandishi wanaosifika nchini Iraq kutokana na uhodari wa kazi zake.

Katika taarifa yake, Mkurugenzi huyo amesema kuwa mwandishi Muwaffak al-Ani ataendelea kukumbukwa daima kwani alitumia muda wake mwingi akiitumikia taaluma yake kwa maslahi ya wananchi.

Amesema kuwa wananchi wa Iraqwataendelea kumkosa na kumkumbuka kwani alikuwa mwanga katika taifa lililoanza kuchomoza baada ya kuzongwa na kipindi kirefu cha migogoro na machafuko.

Muwaffak al-Ani alianza kujishughulisha na uandishi wa habari mnamo mwaka 1962 akianzia katika radio Baghdad alikofanya kazi kwa miaka kadhaa na baadaye akajiunga pia na vituo vya televisheni. Baadaye pia alijihusisha na utoaji mafunzo ya uandishi wa habari

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, Muwaffak al aliuwawa pamoja na kaka yake na watu wengine kadhaa wakati bomu lililokuwa kwenye gari lilipolipuka nje ya msikiti wa Mansour ulioko magharibi mwa Baghdad. 

Muwaffak al-Ani anakuwa mwandishi wa tatu kuuliwa katika kipindi cha miezi 12 nchini Iraq.