UM walaani ubakaji na uhalifu mwingine mashariki mwa DRC

8 Mei 2013

 Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa inasema kulikuwepo na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kwenye jimbo la Kivu Kaskazini nchini humo mwezi Novemba mwaka jana wakati wa mapigano kati ya jeshi la serikali na waasi wa kundi la M23 na huko Kivu Kusini wakati vikosi vya serikali vilipokuwa vikirudi nyuma wakati wa mapambano. Ripoti ya George Njogopa inafafanua zaidi.

 

(TAARIFA YA GEORGE NJOGOPA)

Ripoti iliyotolewa na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imebainisha madhira yanayowakumba wananchi kwenye eneo hilo, ikiwemo yale ya ubakaji wa halaiki, mauwaji pamoja na mateso ya kinyama.

Ripoti hiyo imesema kuwa watekelezaji wa matukio hayo wamekuwa wakiyafanya kwa kupanga na imewatuhumu waasi wa FAEDC ambao walijiondoa kutoka katika miji ya Goma na Sake iliyoko Kaskazini mwa jimbo la Kivu na baadaye kujiunda upya katika mji wa Minova ulioko Kivu Kusin.

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu Navi Pillay amesema kuwa wahusika wa uhalifu huo wanapaswa kujua kuwa mkono wa sheria utapita juu yao na kuongeza kuwa wananchi wa Congo wamepitia vipindi vigumu vya unyanyaswaji na mateso makubwa.

Uchunguzi uliofanywa na maafisa wa Umoja wa Mataifa umebaini kuwepo kwa matukio 135 ya unyanyasaji wa kingono ambao umefanywa na waasi hao katika maeneo ya mji wa Minova.Waathirika wa vitendo hivyo ni pamoja na wasichana 33 wanaokadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 6 hadi 17.