Biashara inayojali mazingira inahitajika kwa maendeleo endelevu: UNEP

8 Mei 2013

Kuendeleza biashara inayojali mazingira ni hatua muhimu ya kufikia maendeleo endelevu, na nchi zinazoendelea zipo kwenye nafasi nzuri ya kuchagiza mabadiliko hayo, imesema ripoti mpya ya Shirika la Mpango wa Mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP.

Ripoti hiyo iitwayo, Uchumi unaojali mazingira na Biashara, inatathmini sekta sita za kiuchumi, zikiwa ni kilimo, uvuvi, misitu, uzalishaji wa viwanda, nishati mbadala na utalii, na ambazo zina nafasi za biashara, na inatambua hatua zinazoweza kuchukuliwa, kama vile mabadiliko ya kisera na utoaji wav yeti, na ambazo zinaweza kuzisaidia nchi zinazoendelea kunufaika kutokana na biashara masoko ya kimataifa ya bidhaa na huduma endelevu.

Mkurugenzi Mkuu wa UNEP, Achim Steiner, amesema katika ulimwengu wa sasa, kuendeleza biashara inayojali mazingira kuna changamoto nyingi, lakini pia kunatoa fursa nyingi muhimu. Ameongeza kuwa ikiwa tunataka kusitisha uharibifu wa bayo anuai, kupunguza uvushaji wa gesi chafu na kulinda udongo na mabahari yetu, ni lazima biashara ya kimataifa iwe endelevu na kuchangia kulinda mtaji wa mali ya asili ya chumi zinazoendelea.