Somalia yahitaji kuungwa mkono ili iweze kusonga mbele: Eliasson

7 Mei 2013

Mkutano kuhusu mustakhbali wa Somalia umeanza hii leo mjini London, Uingereza ambapo Umoja wa Mataifa umeuona ni fursa ya kipekee ya jumuiya ya kimataifa kuonyesha mshikamano na Somalia na wananchi wake katika kujenga amani ya kudumu. Mkutano huo pamoja na mambo mengine unaangalia changamoto za usalama, uwajibikaji wa matumizi ya fedha na haki za kiraia. Joseph Msami na maelezo zaidi.

(TAARIFA YA MSAMI)

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan [YAN] Eliasson anashiriki mkutano huo ambapo amesema mwaka mmoja tangu kufanyika kwa mkutano kama huo, Somalia imepita mchakato wa kisiasa na sasa kinachoangaliwa ni jinsi ya kusaidia serikali ya nchi hiyo kusukuma mbele ajenda ya amani, umoja na ujenzi wa taasisi muhimu.

Amesema wananchi wa Somalia, taasisi za kikanda, jumuiya ya kimataifa zilijitoa kwa hali na mali kufanikisha hali ya sasa na kwamba kinachotakiwa hivi sasa ni mambo matatu.

Mosi Mchakato wa kisiasa unaojumuisha makundi yote, na amepongeza serikali kwa ushirikishaji wa makundi yote nchini humo. Pili nchi jirani kuendeleza mahusiano na ujirani mwema akipongeza taasisi kama vile IGAD na tatu umoja miongoni mwa jumuiya ya kimataifa katika usaidizi wa Somalia. Kuhusu usalama amesema Somalia inapaswa kujengewa uwezo ili hatimaye iweze kusimamia suala hilo bila usaidizi wa kigeni.

Nchini Tanzania, mmoja wa raia wa kisomali aitwae Nawal amesema kile ambacho wanataka kifanyike.

(SAUTI NAWAL)

Naibu Katibu Mkuu alitumia fursa hiyo kumtambulisha mwakilishi mpya wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia Balozi Nicholas Kay anayechukua nafasi ya Balozi Augustine Mahiga ambaye anahitimisha jukumu hilo mwezi ujao.