Katibu Mkuu awa na mazungumzo na Rais Park Geun-hye wa Korea Kusini

6 Mei 2013

Katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa hii leo Katibu Mkuu Ban Ki-Moon amekuwa na mazungumzo na Rais Park Geun-hye ambapo wamezungumzia masuala mbali mbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, malengo ya maendeleo ya milenia, haki za binadamu na hali ilivyo huko Rasi ya Korea.

Mathalani kuhusu malengo ya maendeleo ya Milenia, Bwana Ban ameeleza imani yake juu ya Korea Kusini kutumia uwezo na uzoefu wake katika kuchagiza kufikiwa kwa malengo hayo katika nyanja za elimu, nishati na afya na kusifu hatua ya nchi hiyo ya kuamua kuongeza misaada ya maendeleo kwa nchi za kigeni licha ya hali ngumu ya kiuchumi.

Bwana Ban na Rais Park pia walijadili hali kwenye rasi ya Korea na kumpongeza kiongozi huyo kwa hatua thabiti lakini za kimakini alizochukua wakati wa chokochoko za hivi karibuni za Korea Kaskazini na kuunga mkono uamuzi wake wa kumaliza tofauti kwa njia za mashauriano na kuaminiana.