Vietnam kuwa na kituo cha kufundisha wajasiriamali

6 Mei 2013

Nchini Vietnam, makubaliano yametiwa saini kati ya nchi hiyo na shirika la Umoja wa Mataifa la biashara na viwanda, UNCTAD kwa ajili ya kuanzisha kituo cha 34 duniani cha kuwasaidia wajasiriamali. Ripoti ya Jason Nyakundi inafafanua zaidi.

(RIPOTI YA JASON NYAKUNDI) 

 Vietnam imetia sahihi makubaliano na maafisa wa  UNCTAD kubuni kituo ambacho kitawapa ujuzi wafanyibiashara na ambacho kitakuwa kituo cha kwanza cha aina hiyo baraniAsia.

Akizungumza wakati wa kusainiwa kwa makubaliano hayo mkurugenzi wa Shirika la biashara nchini Vietnam Do Kim Lang amesema  kuwa lengo kuu ni kuhakisisha kumepatikana takriban wataalamu watano wa masuala ya biashara kwa kila mkoa ifikapo mwaka 2015.

Mpango wa pamoja wa malengo ya maendeleo ya milenia umeiruhusu Vietnam kuzisadia familia 4500  zinazotegemea kilimo na kazi za mikono kwenye mikoa minne ya kaskazini mwa nchi.

Chini ya mpango uliongo’a nanga mwaka 2010 jumla ya warsha kumi kuhusu biashara zimeandaliwa nchini Vietnam ambapo jumla ya washiriki 207 wanaopania kuwa wanabiashara wakiwa wamehudhuria mafunzo hayo.

Mpango huo ulioanza kutekelezwa mwaka 1998 umewapa mafunzo zaidi ya wanabiashara 300,000 kupitia uungwaji mkono wa UNCTAD kwenye nchi zinazoendelea. Wanaohitimu wamefanikiwa kupanua biashara ndogo na kubuni maelfu ya nafasi za ajira.