Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 4.6 waathirika na machafuko CAR:OCHA

Watu milioni 4.6 waathirika na machafuko CAR:OCHA

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA linasema mgogoro wa kisiasa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati umesababisha kuzorota zaidi kwa hali ya kibinadamu na kuathiri watu wote milioni 4.6 wa nchi hiyo.

Kutokuwepo kwa taratibu na sheria kumechangia ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwemo mauaji ya kulenga, ubakaji, utesaji, kukamatwa kiholela na uingizaji wa watoto jeshini. OCHA inasema tangu Desemba mwaka jana zaidi ya watu 173, wamekuwa wakimbizi wa ndani huku wengine 49,000 wakikimbilia kutafuta hifadhi katika nchi za jirani.

Kutokana na usalama mdogo imeelezwa kuwa vigumu kwa watoa misaada kufikisha kwa watu wanaoihitaji. Mashirika ya Umoja wa mataifa na NGO’S wanajitahidi kutoa msaada katika mazingira magumu, wamekuwa wakitio msaada wa dawa za kusafisha maji, tembe mbalimbali, na vifaa vya upasuaji katika vituo vya uzazi na hospitali mjini Bangui.

Hata hivyo OCHA inasema fedha zaidi zinahitajika haraka ili kununua vifaa na kuyawezesha mashirika ya misaada kufikisha msaada unaohitajika. Huduma za anga za Umoja wa Mataifa zinahitaji fedha ili kuweza kufikisha misaada katika maeneo ya vijijini ambayo hayafikiki kwa njia ya barabara. Hadi kufikia Mai pili ni asilimia 26 tuu ya fedha zilizoombwa kwa ajili ya CAR ndizo zilizopatikana.