Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatimaye kuna matumaini ya amani DRC: Bi Robinson

Hatimaye kuna matumaini ya amani DRC: Bi Robinson

Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa katika nchi za ukanda wa Maziwa Makuu, Mary Robinson, ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa kuna matumaini makubwa zaidi sasa ya kupatikana amani na utulivu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, DRC, kufuatia makubaliano ya mkakati wa ushirikiakno wa amani na usalama kwa ajili ya nchi hiyo, ambayo yalitiwa saini mwezi Februari mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Akilihutubia Baraza hilo kwa njia ya video, Bi Robinson ambaye ameikamilisha ziara ya wiki nzima katika nchi za ukanda wa maziwa makuu, amesema ametiwa moyo na viongozi wa nchi hizo katika mazungumzo nao, kwa kujitolea kwao kuhakikisha kuwa mkakati wa amani na usalama kwa ajili ya DRC unatekelezwa.

Amesema katika mkakati huo ambao ameuita wa matumaini, kuna nafasi ya kujiepusha na matukio kama yale ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda, na kuleta amani, usalama na maendeleo kwa ukanda wa Maziwa Makuu na watu wake.

(SAUTI YA ROBINSON)

“Sasa ndio wakati wa kugeuza ahadi za mkakati huo kuwa vitendo kamili kwa ajili ya amani. Hakuna hakikisho kuwa mkakati huu mpya wa amani utafanikiwa. Hata hivyo, ni dhahiri kuwa usipofanikiwa, madhara yake yatakuwa mabaya mno. Utahitaji msururu wa vitendo na hatua dhati katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa. Utahitaji kufanya mambo kwa njia tofauti, na nzuri zaidi, na bila kukoma hadi kazi ihitimishwe.”

Bi Robinson amesema sasa kuna nafasi ya kuchukua hatua zaidi kuliko kuitikia tu madhara ya migogoro. Amewaambia wanachama wa Baraza la Usalama pia anapanga kufanya tena ziara katika ukanda wa Maziwa Makuu mwishoni mwa mwezi huu wa Mei.