Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Leo ni siku ya usafi wa mikono duniani, WHO yatoa angalizo

Leo ni siku ya usafi wa mikono duniani, WHO yatoa angalizo

Wakati leo ni siku ya usafi wa mikono duniani, Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO limesema maambukizi yatokanayo na uchafu wa mikono ya wahudumu wa afya yanaendelea kusababisha vifo.

WHO inasema mikono safi ya watoa huduma za afya pamoja na wagonjwa ni muhimu katika kudhibiti maambukizi hayo ambayo ni pamoja na yale ya njia ya mkojo, numonia na uambukizi katika mfumo wa njia ya damu.

Mathalani WHO inasema kwa kila wagonjwa 100 wanaolazwa hospitalini saba  kwenye nchi zilizoendelea na 10 kwenye nchi zilizostawi  wanapata maambukizi ya magonjwa. Na miongoni mwa wanaolazwa kwenye vyumba mahututi idadi hiyo inapanda hadi karibu watu 30 kwa kila watu 100.

Hata hiyo WHO imesema zaidi ya nusu ya maambukizi hayo yanaweza kuzuiwa ikiwa wauguzi wanaweza kuosha mikono wakati wa kuhudumia wagonjwa.

Benedetta Allegranzi, ni afisa kutoka mradi wa WHO wa huduma safi na salama kwa wagonjwa na hapa anataja mazingira ambayo ni muhimu kwa watoa huduma kunawa mikono yao kwa maji na sabuni.

 (SAUTI- Benedetta-WHO)

“Maeneo haya ni kabla ya kumgusa mgonjwa, kabla ya upasuaji, baada ya kushika majimaji ya mwilini, baada ya kumgusa mgonjwa na baada ya kushika mazingira yoyote yale ya mgonjwa.”

 Na akawa na ushauri kwa wagonjwa.

 (SAUTI – Benedetta-WHO)

“Tunaamini kwa dhati kabisa kuwa wagonjwa na familia zao wanaweza kuwa na mchango katika tiba salama. Mathalani kwa kumuomba mhudumu wa afya anayetaka kuwahudumia kunawa mikono yao kabla ya kufanya hivyo, au kuwashukuru pindi wanapofanya hivyo.”

Siku ya usafi wa mikono duniani ilianza kuadhimishwa mwaka 2009.