Waandishi wa habari waachwe wafanye kazi zao kwa uhuru:UM

3 Mei 2013

Leo ni siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani ambapo Umoja wa Mataifa umesema bado mazingira kwa waandishi wa habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari ni hatarishi licha ya kwamba kazi wanayofanya ni muhimu kwa maendeleo endelevu.

Ujumbe wa siku hii ni Zungumza bila hofu na uhuru wa kujieleza kupitia vyombo vyote, lakini shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO linasema licha ya kwamba vitisho dhidi ya wanahabari vinafanyika lakini wanaofanya vitendo hivyo hawakumbani na mkono wa sheria.

Phillipe Kridelka Mkurugenzi wa UNESCO ofisi ya New York akizungumza katika mashauriano maalum kati ya Umoja wa Mataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali mjini New York yaliyoandaliwa mahsusi kwa siku ya Uhuru wa vyombo vya habari alieleza…

(SAUTI Kridelka) (CUT-Kridelka)

“Matukio Tisa kati ya Kumi ya uhalifu dhidi ya wanahabari, wafanyakazi wa vyombo vya habari na waandaaji wa vipindi hayachukuliwi hatua yoyote. Hii haikubaliki. Ghasia na ukwepaji sheria vinakandamiza haki ya msingi ya uhuru, na vinamomonyoa imani ya umma kwa utawala wa sheria. Vitendo hivyo vinahamasisha udhibiti usio na maana na vinaharibu utawala bora.”

Peter Launsky-Tieffenthal ni Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Idara ya mawasiliano ya umma, akizungumza katika mashauriano hayo alisema uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza ni uhuru wa kimsingi na hutoa fursa kwa watu kueleza matarajio yao.

Amesema fursa hiyo ina maana kufichua ukweli na kuupatia umma taarifa za uhakika kutoka vyanzo mbali mbali vya habari huku akifafanua.

(LAUNSKY-TIEFFENTHAL) CUT- Launsky)

“Wanahabari na wafanyakazi wa vyombo vya habari kwa mapana

yake wanahitaji kuwa salama ili waweze kuzungumza na hawapaswi kugharimika kwa kujitoa mhanga ili waweze kutoa taarifa za ukweli ambazo ni muhimu kwa jamii zao.”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud