Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pillay asikitishwa na ghasia za mara kwa mara Papua (Indonesia)

Pillay asikitishwa na ghasia za mara kwa mara Papua (Indonesia)

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Navi Pillay ameelezea hofu kubwa kuhusu ukatili dhidi ya waandamanaji kwenye jimbo la Papua nchini Indonesia tangu Aprili 30.

Askari polisi katika eneo hilo wameripotiwa kutumia nguvu zilokithiri wakati wanapowatia mbaroni watu wanaopeperusha bendera za kutaka kujitenga.

Pillay amesema matukio hayo ni mifano ya ukandamizaji unaoendelea wa uhuru wa kujieleza na matumizi ya nguvu kupindukia.

Ametoa wito kwa serikali ya Indonesia kuwaruhusu maandamano ya amani na kuwachukulia wanaohusika katika ukiukaji wa haki za binadamu hatua za kiesheria.

Duru za habari zinaonesha kuwa mnamo Aprili 30, polisi waliwafyatulia risasi na kuwaua waandamanaji wawili katika mji wa Sorong, ambao walikuwa wanajiandaa kuadhimisha miaka 50 ya Papua kuwa sehemu ya Indonesia, huku waandamanaji 20 wakikamatwa katika miji ya Biak na Timika mnamo Mei1.