Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali, kampuni, wahalifu wazidi kutishia maisha ya wanahabari: Ban

Serikali, kampuni, wahalifu wazidi kutishia maisha ya wanahabari: Ban

Maisha ya waandishi wa habari yanazidi kuwa hatarini na wanaowatisha hawachukuliwa hatua, hiyo ni sehemu ya ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon kwa siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani kesho Mei Tatu akisema kuwa mwaka jana pekee waandishi wa habari 120 waliuawa.  Amesema mwandishi wa habari awe wa radio, televisheni, gazeti au bloga anazidi kukumbwa na vitisho siku hadi siku na hivyo kunyima watu uhuru wa kujieleza ambao ni haki ya msingi kwa mujibu wa tamko la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa. Katibu Mkuu amesema uhuru wa kujieleza ni msingi wa utawala bora, maendeleo endelevu na hata amani na usalama wa kudumu duniani lakini bado inashuhudiwa serikali, kampuni, wahalifu wakitishia waandishi wa habari na hofu yake ni kwamba wengi wao hawachukuliwi hatua zozote.  Amesema ujumbe wa mwaka huu Zungumza bila hofu na uhuru wa kujieleza kupitia vyombo vyote, unatoa fursa ya kuchukua hatua ya kuzingatia haki ya waandishi wa habari kufanya kaziyao muhimu bila hofu.  Bwana Ban amesema Umoja wa Mataifa umeanzisha mpango wa kuhamasisha na kuchukua hatua thabiti za kuweka mazingira huru na salama kwa waandishi wa habari kufanya kazi yao na ametaka kila mtu kuahidi kutekeleza hilo kwa maslahi ya dunia nzima.