Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwa ushirikiano, migogoro yaweza kuzuiliwa: Ban

Kwa ushirikiano, migogoro yaweza kuzuiliwa: Ban

Hatua za kuzuia migogoro zinaweza kupata ufanisi tu pale jamii ya kimataifa inapoongea kwa sauti moja. Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, wakati wa tukio la kuzindua Mhadhara mashuhuri wa Andrew Carnegie kuhusu uzuiaji wa migogoro, kwa heshima ya Dr. David Hamburg.

Bwana Ban amemsifu Dr. Hamburg kwa mchango wake kwa ulimwengu na Umoja wa Mataifa katika nyanja mbalimbali, zikiwemo afya ya umma, elimu, kuzuia uenezaji wa zana za nyuklia, na hususan katika kuzuia migogoro.

Wakati wa mhadhara huo ambao umetolewa mjini New York Jumatano jioni, Bwana Ban amesema aghalabu juhudi za kutekeleza diplomasia ya kuzuia migogoro hukumbana na vizuizi vya hofu kuhusu uhuru wa nchi wanachama na kuogopa kuingiliwa mambo ya ndani ya nchi na wageni.

Ameongeza kuwa migawanyiko katika Baraza la Usalama au katika mitazamo ya mashirika mbalimbali inaweza kufanya kazi ya wapatanishi kuwa ngumu.