Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya misaada yataka kusita kwa bomoabomoa na upanuzi wa makazi ya Walowezi:

Mashirika ya misaada yataka kusita kwa bomoabomoa na upanuzi wa makazi ya Walowezi:

Mashirika 16 ya misaada na maendeleo yanawataka viongozi wa dunia kuishinikiza Israel kukomesha mara moja bomoabomoa ya nyumba za wapalestina na kujenga makazi ya Walowezi wa Kiyahudi baada ya bomoa bomoa ya karibuni kuwaacha Wapalestina 52 bila makao.

Kati ya April 23 hadi 30 mwaka huu mabulidoza ya Israel yamesambaratisha makazi na majengo 36 ya Wapalestina, yakijumuisha makazi matano ya dharura ambayo yalitolewa na ubalozi wa Ufaransa kwa ajili ya familia zilizoachwa bila makazi na bomoa bomoa ya Israel mapema mwaka huu.

Bomoa hiyo ni katika eneo zima la Ukingo wa Magharibi , maeneo ya karibu na mkazi haramu wa Walowezi, au maeneo ya kijeshi ya Israel ,maeneo ambayo yanadhibitiwa kijeshi na kiraia na serikali ya Israel.

Mashirika hayo yanasema viongozi wa dunia wana jukumu la kuiwajibisha Israel kwa upanuzi wa kamazi ya Walowezi, ubomoaji wa makazi na majengo ya Wapalestina na kuwahamisha kwa nguvu, mambo yote ambayo yanakiuka sheria za kimataifa.

Maelfu ya Wapalestina wanaishi kwa vitisho vya kusambaratishwa. Jana pekee majeshi ya Israel yamezisambaratisha familia 70 za Kipalestina kutoka katika vijiji sita iki waendeshe mafunzo yao ya kijeshi.